1 Kings 21

Shamba La Mizabibu La Nabothi

1 aBaada ya hayo, Nabothi, Myezreeli, alikuwa na shamba la mizabibu jirani na jumba la kifalme la Ahabu mfalme wa Samaria. 2Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilitumie kwa bustani ya mboga, kwa kuwa liko karibu na jumba langu la kifalme. Badala yake, nitakupa shamba jingine la mizabibu zuri zaidi au, kama utapenda, nitakulipa kiasi chochote unachoona ni thamani yake.”

3 bLakini Nabothi akamjibu, “Bwana na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”

4 cBasi Ahabu akaenda nyumbani, mwenye huzuni na hasira kwa sababu ya yale ambayo Nabothi, Myezreeli, alikuwa amesema, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.

5Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”

6Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi, Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au kama ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ”

7 dYezebeli mke wake akasema, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme katika Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupatia shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”

8 eKwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu akaweka muhuri wake juu ya hizo barua, akazipeleka kwa wazee na kwa watu wenye cheo walioishi katika mji pamoja na Nabothi. 9Katika barua hizo aliandika:

“Tangazeni siku ya watu kufunga na mkamketishe Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu.
10 fLakini waketisheni watu wawili wabaya kabisa mkabala naye, nao washuhudie kuwa yeye amemlaani Mungu na mfalme. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”

11Hivyo wazee na watu wenye cheo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua aliyowaandikia. 12 gWakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu. 13 hKisha watu wawili wabaya kabisa wakaja wakaketi mkabala naye, nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa. 14Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”

15 iMara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na uchukue lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.” 16Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka na kushuka ili kulichukua shamba la mizabibu la Nabothi.

17Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, Mtishbi: 18“Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambapo amekwenda alimiliki. 19 jUmwambie, ‘Hivi ndivyo Bwana asemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’ ”

20 kAhabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!”

Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kufanya uovu mbele ya macho ya Bwana.
21‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kutoka kwa Ahabu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, wa mtumwa au wa mtu huru. 22 lNitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ile ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kuwa umesababisha Israeli kutenda dhambi.’

23 m“Pia kwa habari ya Yezebeli Bwana anasema, ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’

24 n“Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”

25(Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni mwa Bwana, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe. 26 oAlitenda kwa uovu sana katika kuabudu sanamu, kama wale Waamori ambao Bwana aliowafukuza mbele ya Israeli.)

27 pAhabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.

28Ndipo neno la Bwana lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, 29 q“Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

Copyright information for SwhNEN